TAMKO LA TAASISI ZA KIISLAMU KUHUSU KUVUNJWA KWA MUHADHARA DONGE

19 JUN, 2012

 BISMILLAH RAHMANI RAHIM

TAMKO LA JUMUIYA NA TAASISI ZA KIISLAMU ZANZIBAR

Kila sifa njema anastahiki ALLAH (S.W.T), Rehma na Amani zimuendee Mtume Muhammad (S.A.W), watu wake, Maswahaba zake na walio wema katika Uislamu.

Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar baada ya kufuatilia kwa hatua za awali na kufanya tathmini ya hali ya mambo namna ilivyotokea tarehe 17 juni, 2012 inatoa tamko RASMI kama ifuatavyo:

Siku ya tarehe 17 juni, 2012 majira ya saa nane na nusu za mchana waislam waliondoka viwanja vya malindi eneo la mjini magharibi na msafara wa gari, vespa na Pikipiki ukielekea kwenye muhadhara Kaskazini Unguja eneo la Donge sambamba na wenzao wengine waliotoka mashamba yote ya Unguja kuelekea hukohuko Donge katika Msikiti uliopo eneo  linalojulikana kwa jina la Donge pwani, tulipofika Mahonda msikiti wa Ijumaa ambao upo karibu na kituo cha polisi cha mahonda, majira ya saa tisa na dakika kumi jeshi la polisi lililovalia sare za askari wa FFU liliwazuia wananchi hao kuendelea na safari yao ya Donge nakusababisha mkusanyiko usio wa lazima.

Watu waliokuwa katika msafara huo walilazimika waingie msikitini huku wakisubiri viongozi wao wa jumuiya na taasisi za kiisilamu wawaongoze, wakati viongozi wa jumuiya na taasisi za kiisilamu walipofika eneo hilo walitoka kwenye gari ili kwenda kufanya mazungumzo na askari, ndipo FFU walipoaza kurusha mabomu ya machozi ovyo na kuwatawanya waumini hao, huu ni uvunjaji wa katiba zote mbili na ukiukwaji wa haki ya raia na uhuru wake wa kuabudu kama inavyoelezwa na katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kifungu cha 19 (2) ambayo inasema “Kazi ya kutangaza dini, kufanya ibada, kueneza dini itakua huru na jambo la hiari ya mtu binafsi na shughuli na uendeshaji wa jumuiya za dini zitakua nje ya shuguli za mamlaka ya nchi…” rejea pia katiba ya Jamhuri ibara. 19 (1), (2), (3).

Pia kufanya hivyo ni kwenda kinyume na katiba ya Zanzibar ibara ya 16 (1) kwa kuwazuwia watu kwenda watakapo ndani ya Zanzibar…, sheria kama hii pia inaelezwa ndani ya katiba ya Jamhuri…

Ibara ya 17(1) inatamka wazi kwamba “…Kila raia wa Jamhuri ya Muungano anayo haki ya kwenda kokote katika Jamhuri ya Muungano…”. Pia kifungu kidogo cha (2) (b)(i),(ii),(iii) vimetoa maelezo zaidi.

Jeshi la Polisi limekwenda kinyume na kifungu cha  18 (1) cha sheria ya Zanzibar kwa kuzuwia uhuru wa maoni Sambamba na Kwenda kinyume na Sheria ya mwaka 1977 ya Jamhuri ya Tanzania ibara ya 18 (1) “…kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake, na kutafuta, kupokea na kutoa habari…”

Isitoshe, juu ya ukiukwaji wote huo askari hao wamefanya unyama na uhalifu wahali ya juu kwa kuunajisi Msikiti wa Ijumaa wa Mahonda kwa kuwahujumu Raia wasio na silaha ndani ya Msikiti kwa kuwarushia mabomu ya machozi yasiojulikana idadi yake ambapo hadi hii leo msikiti huo hausaliki ndani kutokana na harufu kali ya mabomu. Pia askari hao walipiga risasi pamoja na kuingia ndani ya Msikiti na viatu na kuvunja kwa makusudi vyombo (Vespa, Pikipiki, Baskeli n.k) vilivyoegeshwa eneo la msikiti huo wa Ijumaa.

Sambamba na hilo, polisi wamevunja taa ya mbele na nyuma ya vespa ya mwandishi wa  habari wa jumuiya pamoja na taa za gari inayobeba vifaa vya mihadhara kichuki baada ya kuikamata mapema tu na kuifikisha polisi, hali hii ilitokea wakati gari ikiwa kituoni chini ya kizuizi cha polisi baada ya kuikamata tokea saa saba nanusu za mchana kabla ya kufika kwa misafara inayokwenda kwenye mihadhara hadi leo hii gari hiyo inashikiliwa na polisi kituoni mahonda.

Pia katika jumla ya matukio ni kuandamwa na kufukuzwa kwa gari ya kiongozi wa Jumuiya ya Maimamu Sh. Farid Hadi Ahmed yenye Namba ya usajili Z 628 DJ aina ya NISAN X-TRAIL iliyofukuzwa kwa pikipiki inasadikiwa na watu ambao walitumwa na jeshi la polisi kwa lengo la uhalifu dhidi ya Amir Farid kitendo ambacho kilisababisha  ajali ya kupinduka  kwa gari hiyo na kusababisha kujigonga na mti huko Dole tukio ambalo liliripotiwa kituo cha polisi cha Muembe Mchomeke. Haya yote yaliyofanywa na Jeshi la Polisi kuwajeruhi watu wasiokua na hatia pamoja na kuharibu mali  yanakwenda kinyume na katiba na sheria za nchi.

Jambo la kushtusha zaidi ni kitendo cha kuwadhililisha wanawake na kufikia hadi kuwakashifu kwa kuwachania nguo zao na kuwavua mashungi yao pia hata watoto wadogo mitaani wako walopata kipigo, kitendo cha  kuwatimba wanawake kwa viatu bila ya huruma na kuwapiga marungu na kuwajeruhi vibaya sehemu za usoni na mwilini kwa ujumla, huo wote ni unyama na ukiukwaji wa haki za binaadamu.

Ilipofikia wakati wa laasiri jeshi la polisi walianza pia kupiga mabomu ndani ya msikiti wa donge pwani pamoja na kuuhujumu msikiti na waumini wakiwa wanaswali katika msikiti wa Donge skuli na kuvunja vioo vya msikiti huo, huu wote ni udhalilishaji wa dini ya Kiislamu pamoja na waumini katika eneo hilo.

Vile vile, askari wa jeshi la polisi walikata kwa visu mipira ya vyombo vya wananchi kama vile vespa na baskeli zilizokua zimeegeshwa msikitini hapo na askari hao walivunja heshma ya msikiti kwa kuingia na viatu ndani ya misikiti hiyo.

Sambamba na hilo,  walimkamata mzee Kassim Shekha mwenye Umri wa miaka 50 aliekua akiswali swala ya laasir walimjeruhi vibaya miguuni kwa mlipuko wa bomu la machozi akiwa ndani ya swala, pia kijana Othman Ali (22) aliamriwa aingie Msikitini na hatimae kujikuta akipigwa kwa mateke, vibao na kuchaniwa nguo huku akiamriwa lazima atembee kwa magoti pamoja na wenziwe hadi kituoni Mahonda.

Kwa taarifa tulizozipata kutoka kwa kamishna wa jeshi la polisi Zanzibar kupitia vyombo mbali mbali vya habari ikiwemo gazeti la serikali la Zanzibar leo toleo nambari 3789 la tarehe 18 Juni, 2012 lilisema likimnukuu Kamishna huyo ndugu Mussa Ali Mussa eti hakuna alie jeruhiwa wakati taarifa za kuaminika zimeripoti watu thalathini na nne ambapo wanaume ni 27 na wanawake 9. Upotoshaji huo wa jeshi la polisi ni kuonesha namnagani jeshi la Polisi lisivyo wajali wananchi, roho na mali zao na jinsi linavyopotosha ukweli wa mambo. Pia kutokujali hata kwenda kinyume na viapo vyao vya uaminifu wanapoingia kwenye ajira, Kwa kiongozi wa Jeshi la Polisi kwa nafasi kama hiyo ya kamishna alipaswa awe mfano mzuri kwa walio chini yake.

Matukiyo yote hayo ya kunajisi Misikiti na kudhalilisha waumini wakiwa ndani ya nyumba za ibada yanazidi kujenga imani kua ni kweli yale yanaosemwa kua jeshi la Polisi linahusika kwa njia moja au nyengine katika suala zima la unajisi na uchomwaji wa Makanisa kiushiriki na ufichaji wa wahalifu kisha kutoa taarifa za uongo na  kuwafanya Waislamu ndio chaka lao.

Baada ya hayo machache yaliyotangulia hapo juu pamoja na kukutana na waathirika na wananchi wa Donge, Jumuiya na Taasisi za Kiislamu inatamka kwamba:

  1. Jumuiya inasikitishwa sana na taarifa za uongo zisizo kuwa na ukweli na inalitaka jeshi la polisi na Vyombo vyote vya Dola wafanye kazi zao kwa ukweli na uaminifu kama wanavyotakiwa kwa mujibu wa muongozo wa haki za binadamu wakitambuwa umuhimu wa jukumu lao la kutunza amani na utulivu na jukumu la kutoingilia haki za watu. Kila mtu anayo haki ya kuwekewa mazingira muafaka ya kitaifa na kimataifa yatakayomuwezesha kupata haki zake za binadamu. Kwa maana hiyo tunalitaka jeshi la polisi litueleze kwa katiba gani na sheria ipi iliyotumika kuzuia uhuru wa kuabudu na kutoa mihadhara na kukusanyika waumini wa kiisilamu misikitini? Tunavyofahamu sisi jumuiya, ni kuwa jeshi la polisi na vyombo vingine vya dola wana jukumu la kuheshimu, kulinda na kutetea haki za binadamu kwa watu wote bila ya ubaguzi.
  2. Wananchi wa Donge wanasema wamechoshwa na ubaguzi na udikteta wa Shamhuna na wanaitaka serikali ya umoja wa kitaifa kupitia baraza la wawakilishi itoe ufafanuzi wa wazi kabisa, ni kwa sheria gani wananchi wa Donge wananyimwa fursa ya kufaidi uhuru wa kuabudu na uhuru wa maoni pamoja na uhuru wa kuchanganyika na ndugu zao wazanzibari? vile vile haki ya kutumia TV na DVD zao mitaani uhuru ambao unaingiliwa na masheha kwa kuwazuia watu kutizama watakacho na kufikia hadi kuwatisha kuwapeleka Polisi na hata kuwanyang’anya mali hizo jambo ambalo linaweza kusababisha uvunjifu wa amani wakati inafahamika kuwa haki zote hizo zinalindwa na katiba ya Zanizbar kwenye ibara zifuatazo 17, 18, 19 na 20.
  3. Wananchi wa Donge pia wanomba ufafanuzi kutoka baraza la wawakilishi kwani kwa miaka yote wanajiona kuwa wanabaguliwa wakati wananchi wenzao wa mashamba yote mengine  katika wilaya tofauti wakipata haki kikamilifu, jee wao si wazanzibari? Ni dhambi gani waliyotenda hata wakabaguliwa kiasi hicho? Au Donge ni nchi yenye mfalme kama wafalme wa ki-Misri wakijulikana kwa jina la FIRAUNI?
  4. Wananchi wa Donge wanaliomba baraza la wawakilishi tukufu ndani ya siku kumi na nne (14) litoe ufafanuzi wa haki juu ya masuala yao yote, ikishindakana hivyo wasije wakalaumika kwa maamuzi watakayochukua. Pia wanaviomba vyama vyote vya siasa viwe makini sana kuwatetea haki zao.
  5. Jumuiya na taasisi za kiislamu zinawaahidi wananchi wa Donge kuwa ziko tayari kuwaunga mkono kwa maamuzi yoyote watakayo yachukuwa na kuwataka waislamu wote wawe tayari kwa hilo.
  6. Jumuiya za kiisilamu zinawapa pole waathirika wote na kuwapa hongera wazanzibari wote kwa uimara na kutotetereka katika kudai haki zao pamoja na kutoa wito wa kudumisha amani na utulivu, pamoja na kuwa na subra na kutolipiza kisasi.

Mwisho, Jumuiya na Taasisi za Kiislamu zinapenda ifahamike kwamba, inatoa na kupaza sauti ya ukombozi wa Zanzibar kwa  njia za amani bila ya kutumia nguvu za silaha bali  kwa kutumia nguvu za hoja na inaendesha harakati zake  hizo za ukombozi juu ya misingi ya sheria za nchi na katiba.

Hivyo basi, wananchi wa Zanzibar kudai uhuru wa kujiamulia mambo yetu ni haki yetu ya msingi, na kwa hilo HATUNA MJADALA (MPAKA TUTAKAPOIPATA NCHI YETU INSHA-ALLAH), tutaendelea kudai haki zetu kwa kila hali bila ya kuvunja sheria za nchi.

Tunasisitiza kuendelea na kuidai Zanzibar yetu huru ingawa tunaelewa gharama ya kufanya hivyo ni kubwa ikiwemo kupoteza roho zetu na mali zetu. Na tunatamka wazi yakwamba tumechoka na ukoloni wa watanganyika wachache wasioitakia mema Tanganyika na Zanzibar.

Tutaidai nchi yetu kwa gharama yoyote  mpaka kuipata Zanzibar yetu huru.

“…FREE ZANZIBAR…”

“TUACHIWE TUPUMUE”

WABILLLAH TAWFIQ

 

 

 

About uamshozanzibar

Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislam, Zanzibar

Posted on June 21, 2012, in Uncategorized. Bookmark the permalink. 7 Comments.

  1. mohammed bakar

    Asalamu alykum, wakati umefika sasa kwa wazanzibar kudai nchi yetu dhidi ya dhulma kubwa na ya miaka mingi. tunahitaji kuwa na imani thabiti kwani jambo hili si la mdhaha. wanaendelea kutumia mbinu mbali mbali kuhakikisha kuwa wazanzibar sauti zao hazisikiki. tusirudishwe nyuma na unyama wao na tuwe kitu kimoja na tuhakikishe kuwa tunalinda umoja wetu, kwani lengo lao ni kutugawa sisi waislamu na wazanzibari kwa jumla. sisi wazanzibar tunasema kuwa hatukubali mpaka kieleweke. tumechoka, watuache tupumue.

  2. Wananchi wenzangu wa Zanzibar, tunakuombeni sana msijeb mkatetereka na sisi ndugu zenu tunaosoma huku tuko pamoja nanyi na Insha Allah Mutatuona tuko karibu na likizo,Aidha nichukue fursa hii kuwapa pole na kuwatakia moyo wa subra ndugu zetu wa Donge na tuone kwamba Allah anatutahini tu kutuangalia jee sisi niwakweli?,Nachukua fursa hii pia kuwanasihi na kuwaomba sana waislamu popote walipo katika dunia kulaani uvunjaji huu wa haki za binaadamu ,Mwisho nawaomba wajumbe wa baraza la wawakilishi kufahamu kuwa wao ndio wawakilishi wetu namba moja lisemeeni hili kwa nguvu zenu zote., mwisho kabisa nawaambia ndugu zangu wazanzibari tunaona jinsi gani watu tuliowaamini wanavotufanyia ,hivo basi nijuu yetu kuwa makini na hichi kiwe kipimo tosha cha kuangalia nikiongozi yupi anaweza akatufaa, atakae kwenda kinyume na kutusaliti basi jawabu yake ni kumkataa tu. TUSIVUNJIKE MOYO WATATUACHA TU TUPUMUE KWA UWEZO WA ALLAH.

  3. Tusishangae hata kidogo kwa shamhuna kufanya anayoyafanya,zote ni mbegu za Nyerere alizopanda,Mimi sishangai maana viongozi wetu wengi sijui ni uvivu tu wakusoma maandiko ya historia au ni uamuzi wao tu wa kupuuzia,Yupo mkatoliki mmoja anaitwa Dr. SIVALON, aliandika kitabu chake akakiita “THE DARK SIDE OF NYERERE LEGACY”, bwana huyu licha ya ukatoliki wake wakati anafanya research yake ya Phd, alimueleza nyerere ni nani na ana nia gani, sasa ameshazalisha ,tunao Nyerere hadi Zanzibar ,ndi hao akina Shamhuna.Kipo pia kitabu kiitwacho “MAISHA NA NYAKATI ZA ABDULWAHUID SYKES” nacho kinawaelezea akina Nyerwere,n pia Dr.Mohammed Said katika kitabu chake “KWAHERI UKOLONI KWAHERI UHURU”ameeleza vya kutosha.Waislamu sisi tunayo killa sababu ya kuukataa Muungano na kwa bahati hata wao wanaoona unawafaa hata kuzieleza faida za Muungano hawawezi, kwa mfano tarehe 16/6/2012,wanafunzi wa vyuo vikuu mkoani Morogoro walifanya mkutano wa hadhara wakawaalika viongozi wengi sana akiwemo Mh. Samia (Waziri wa muungano) alipokaribishwa ili kuufahamisha ummah faida za muungano alinifanya nibubujikwe na machozi, Msomi huyu na kiongozi alianza kwa kuwatathmini vibaya UAMSHO,na baadae ndipo akaanza kutaja faida za muungano alisema moja kati ya faida ya muungano nikuwa watanganyika walikuwa wakiwabeza wazanzibari na kuwaita watu wa urojo lakini kwa sababu ya muungano sasa urojo unapikwa hadi Daressalamu,nilidhani labda nimesikia vibaya lakini nikaja kugundua kuwa ndivo hasa alivokusudia baada ya kurudia rudia,hapa nilianza kugundua kitu kuwa viongozi wetu wengi wa[po madarakani kwa faida zao binafsio. Faida ya pili akasema yeye kasoma Mzumbe na lau si Muungano yengebidi asome kwao Zanzibar, hapa pia niligundua kitu kwamba viongozi aidha hawafahjamu historuia ya zanzibar ama hawataki kwa sababu wao wanafaidika. Hivyo basi ni juu yetu wazanzibari kushikamana na kuhakikisha kuwa zanzibar tunaitoa katika makucha haya ya Madhalimu wa ndani na nje.WATATUACHA TUPUMUE KWA UWEZO WA ALLAH”

  4. Nazipongeza jumuiya za Kiislam ZNZ kwa TAMKO lao lenye muamko mzuri juu ya mustakbali wa amani ya nchi yetu ya ZNZ. Kazi ipo kwa ljeshi la Police.

  5. assalamu alayku. mimi ni mwanachuo nipo dar.namshuku allah.s.w.kuwezesha uamsho kupata blog hii ambayo itatuezesha sisi tulio mbali na znz kupata khabari za ukweli na uwazi.naskitika sana kwa kupashwa yalitokea morogoro kwa waziri wa muungano.ila inshaallah mungu atatufungulia minyororo hii ya ukoloni.

    • K wa bahat nzuri kaka mimi npo apa {MUM} Moro na niliudhuria siku iyo, machoni mwagu sikuamini kama kuna mzanzibar anaweza kuongea vle lkn yy kaongea kwa kujiamini. Ama kweli watu ni tofaut sana. nilijiuliza ivi amerubuniwa au amejirubuni mwenyewe?

Leave a reply to Arshad Cancel reply