Ukaidi wa CCM utaiwasha moto Zanzibar

Na Joster Mwangulumbi, MwanaHALISI, 6 Juni 2012

Umma wa Wazanzibari ukiongozwa na Uamsho wanasema Muungano huu sasa basi.

NCHI zilizokubali mageuzi ya kisiasa bila shinikizo zilijiepusha na machafuko au kuwasha moto nchi zao, lakini zilizokataa zilishindwa kuuzima hata kwa mtutu wa bunduki, moto ukaendelea kuunguza nchi nzima kama ilivyo Syria leo.

Hali inayoendelea katika visiwa vya Unguja na Pemba inawataka viongozi wa pande zote mbili za muungano kuondoa blanketi jeusi lililoziba nyuso na fikra juu ya haja ya kuupitia upya muungano nchi isije ikawaka moto utakaoua hata sisimizi wasio na hatia.

Wazanzibari wamezungumza kwa lugha inayoeleweka tangu baada ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar 26 Aprili 1964 lakini walizimwa. Waliokuwa ndani ya uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) walipewa majibu suala hilo linajadilika.

Ukaidi huu una madhara, sauti ya Wazanzibari inasikika vizuri kabisa – hawautaki muungano unaoififisha Zanzibar.

Matakwa ya Wzanzibari ni kuwemo katika muungano ambao Zanzibar itabaki inatambuliwa kama nchi ndani na nje ya muungano. Hicho ndicho wanachosema.

Mwaka 1984 Mwalimu Julius Nyerere alipolitangazia taifa kuhusu kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa Zanzibar alikiri Wazanzibari wa leo wanazungumza, wanabisha; si wale waliokuwa wanakaa wanasikiliza.

Mwaka huo ndio ambao Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ilitia chumvi kwenye kidonda cha kero, ilipomvua urais Aboud Jumbe Mwinyi.

Hata hivyo, akiwa nje ya serikali, miaka 10 baadaye yaani mwaka 1994 Jumbe alitunga kitabu kiitwacho The Partner-ship: Tanganyika-Zanzibar Union : 30 Turbulent Years kilichoeleza malalamiko mbalimbali, kero na kasoro za muungano na namna ya kuzitafutia ufumbuzi.

Katika kitabu hicho Jumbe anahoji makubaliano hayo kama ni kweli ilikubaliwa Tanganyika isiwepo? Kauli na msimamo wake uko bayana haridhishwi na namna mambo yanavyokwenda. Jumbe anataka muungano umilikiwe na watu badala ya kuwa wa viongozi pekee.

Lakini mwaka huo wa 1994 serikali ya CCM, ikafumua katiba na kuanzisha utaratibu wa kuwa na mgombea mwenza wa Rais hivyo kufuta utaratibu wa zamani wa rais akitoka Zanzibar makamu anatoka Bara na rais akitoka Bara basi makamu anatoka Zanzibar.

Maamuzi haya, yanayozidisha kero katika muungano huu yameratibiwa na kutetewa na CCM. Vyama vingine vyote vya siasa kuanzia CUF, CHADEMA, NCCR-Mageuzi na vinginevyo vinataka muungano utakaoiacha Zanzibar ionekane na ibaki huru kufanya shughuli zake katika shirikisho au muungano wa serikali tatu.

Mwaka 2005 kikundi cha wanaharakati kinachojiita G10 kikiongozwa na Rashid Salum Adiy kilifungua kesi ya kikatiba katika mahakama kuu za Zanzibar kikitaka mwansheria mkuu wa Zanzibar awasilishe hati rasmi ya makubaliano ya muungano.

Hiyo yote ilikuwa kutafuta uhalali wa muungano. Lakini hata aliyekuwa mwanasheria mkuu Iddi Pandu Hassan alidai hata yeye hajui ilipo.

Mwaka 2008, watu waliosadikiwa kwamba wanatoka Pemba waliwasilisha waraka kwenye ofisi za Umoja wa Mataifa (UN), Dar es Salaam wakitaka Zanzibar ijitenge.

Waziri mkuu, Mizengo Pinda alipojibu swali bungeni juu ya hadhi ya Zanzibar ndani na nje ya muungano, alishutumiwa vikali na Wazanzibari. Wao wanasema Zanzibar ni nchi yenye mipaka inayoeleweka.

Ibara ya 2, kifungu kidogo cha 1 cha Katiba ya Zanzibar inataja: “Eneo la Zanzibar ni eneo lote la visiwa vyote vya Unguja na Pemba na visiwa vidogo vidogo vilivyovizunguka na bahari yake, ambayo kabla ya Muungano ikiitwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.”

Mwaka 2009, watu wasiojulikana walisambaza katika maeneo mbalimbali kisiwani Pemba vipeperushi vyenye ujumbe wa kuwataka wajitambue.

Desemba 27, 2011, Makamu wa kwanza wa rais na Katibu mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, alieleza kwa uwazi matakwa ya Wazanzibari.

Matakwa hayo aliyoyaweka wazi alipozungumza katika viwanja vya Kibandamaiti ni:

Wananchi visiwani humo kuwa na benki kuu yao kwani kuendelea kutegemea Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kunainyima haki kutekeleza mipango yake ya maendeleo kwa ufanisi.
Uwepo mfumo wenye usawa wa uchaguzi badala ya huu wa sasa uliosbabisha nafasi ya rais wa muungano kubaki bara kwa muda mrefu.

Wakati wa vikao vya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Aprili 2012, kundi la vijana zaidi ya 30 walikusanyika katika viwanja vya Baraza hilo wakitaka kuitishwa kwa kura ya maoni ya kuamua hatima ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliofikisha miaka 48 sasa.

Kiongozi wa kikundi kile alikuwa Adiy ambaye alisema lengo la kukusanyika pale lilikuwa kufikisha ujumbe kwa wawakilishi ambao pamoja na mambo mengine wanahitaji kuitishwa kura ya maoni itakayoamua mustakbali wa nchi yao ambayo imevamiwa na Tanganyika kimabavu.

Mara baada ya kuwasilia katika viwanja hivyo majira ya saa moja kamili asubuhi vijana hao walionekana wakiwa na mabango kadhaa yakiwa na maandishi ya kutaka kura ya maoni kwa kuwa Zanzibar ina sheria ya kuitisha kura ya maoni iwapo kutatokea jambo linalotaka kuamuliwa na wananchi wenyewe.

Kama kawaida, kabla ya kuingia ndani ya viwanja hivyo askari waliokuwepo katika viwanja vya baraza hilo waliwazuwia vijana hao. Punde polisi wengi zaidi walifika kuwadhibiti.

Kwa hiyo, harakati hizi za Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu (Jumuki), ni juhudi nyingine za Wazanzibari kutumia jukwaa jingine, lugha nyingine ili kudai jambo moja tu, “muungano huu upitiwe upya”.

Mwaka jana wakati wa kujadili muswada wa sheria ya marekebisho ya katiba, kiongozi wa Jumuki alichana muswada ule akitaka wapewe kwanza fursa ya kupiga kura ya maoni Wazanzibari waamue kuridhia au kujitoa kwenye muungano.

Viongozi wa kitaifa wanaweza kupeleka polisi wote kudhibiti vurugu zilizofanywa na vijana hadi kufikia kuchoma makanisa, lakini polisi hawawezi kuzima fukuto walilonalo moyoni.

Viongozi wa kitaifa wanaweza kuendelea kupuuza kila lugha inayotumiwa na makundi mbalimbali ya watu, lakini madhara yake ni makubwa wanaweza kutumia “lugha” mbaya zaidi. Kama muungano hautakuwa wa watu, hauwezi kuimarika na hauwezi kuwa wa maana.

Maalim Seif katika ushauri wake alioutoa katika viwanja vya Kibandamaiti alisema, “Utakapofika wakati wa kutoa maoni tusahau itikadi zetu, tuungane kulinda maslahi ya Zanzibar, vyama vya siasa ni taasisi za kupita, ASP haipo, TANU haipo na ZNP haipo, lakini Zanzibar itaendelea kuwepo.”

Ni kweli hata waasisi wa muungano Nyerere na Abeid Amani Karume hawapo, lakini Zanzibar ipo, itabaki na itaendelea kuwepo. Je, kero nazo ziendelee kubaki?

0789 383 979

Advertisements

About uamshozanzibar

Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislam, Zanzibar

Posted on June 10, 2012, in Uncategorized. Bookmark the permalink. 1 Comment.

  1. naamini kumkata simba pua ni ngumu na ndio hivyo hivyo kuuvunja muungano ni vigumu lakini kwa uwezo wa mungu muungano umekwisha.vijana wa zanzibari tujiandaeni kwa wingi kuvaa kombat.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: