Tamko la MUWAZA Kuhusu Kadhia ya Matukio ya Hivi Karibuni Nchini Zanzibar

Mustakbali wa Zanzibar

MUWAZA imesikitishwa na matukio ya hivi karibuni yaliyotokea katika nchi yetu, Zanzibar. Tumeshuhudia hali iliyosababisha upungufu wa utulivu, uharibifu wa mali pamoja na mazingira katika wakati ambao nguvu na umoja wa kuitetea Zanzibar unaendelea kuimarika kwa kasi kubwa. Tukio la matembezi ya ghafla yaliyoongozwa na jumuiya ya UAMSHO lilitafsiriwa kama ni ukiukwaji wa taratibu kwa vile lilijumuisha watu wengi na lilikosa matayarisho ya ulinzi unaostahiki kwa washiriki wake pamoja na sehemu walizopitia. Ni jambo la kushukuru kwamba licha ya upungufu wa matayarisho ya ulinzi huo, matembezi hayo yalimalizika kwa salama bila ya uharibifu wowote.

Hatua ya polisi ya kumtia kuzuizini Sheikh Mussa ilionekana yenye kukosa hekima na yenye mbinu ya udhalilishaji. Kitendo hiki pamoja na nguvu za ziada za kuwatawanya vijana waliokusanyika katika kituo cha polisi, kilionekana kukosa busara na hekima. Ulipuaji mabomu ya machozi wenye athari kubwa kimazingira na binaadamu (hasa katika sehemu za wajawazito na watoto) hakikuonekana kama ni kitu cha busara.

Kuna kila dalili kuwa mtiririko wa matukio haya, umepelekea makundi mengine yenye malengo tofauti na mustakbali wa Zanzibar kuona ni fursa kwao kufanya vitendo viovu na vya kiharibifu aidha kwa kukidhi utashi wao au kutia dosari harakati za jumuiya za Kizanzibari.

Bila ya kutafakari, watu hao walijihusisha na uharibifu wa mali za watu wa kawaida, nyumba za ibada, sehemu za biashara, n.k. Haiwezi kuaminika kwamba wafuasi wa dini wanaweza kuvunja maduka ya ulevi wakaiba na kunywa ulevi huo hadharani. Bila shaka waliofanya vitendo hivyo ni watu hatari sana wenye nia ya kufisidi harakati nzima za kudai mamlaka ya Zanzibar.

Ni lazima tukubali kwamba kuna baadhi ya watu ndani ya Zanzibar ambao bado hawajafurahi na hali ya utulivu na maelewano tuliyonayo. Endapo watu hao wamechoshwa na utulivu tulionao ni vyema wakatekeleza agizo la Rais wetu la kuhama nchi. Maridhiano tuliyonayo ni matunda ya kazi nzito iliyofanywa na viongozi wetu na katu hatuwezi kurudi katika hali ya mtafaruku.

MUWAZA imefarijika kusikia hotuba ya Rais wa Zanzibar juu ya kadhia hii iliyojitokeza hivi karibuni. Ni jambo la matumiani kuona kauli yake imejaa uvumilivu, busara na hekima kubwa. Hotuba yake imekuwa tofauti kabisa na hotuba tatanishi za huko nyuma zilizotolewa na viongozi wengine wa Zanzibar na wa Muungano kabla na baada ya matukio ya hivi karibuni.
MUWAZA ingependa kuona uchunguzi wa kina unafanywa ili kuwapata waliohusika na vurugu zilizotokea na kuwafikisha katika vyombo vya sheria. Uchunguzi huo ni vyema ufanyike kwa uwazi na uadilifu ili kuepuka kubambikiza kesi za kitatanishi kwa wasiohusika.

MUWAZA ingependa kuona Serikali ya Zanzibar inatumia mamlaka yake ya kinchi ili kusimamia suala la utulivu na maelewano kwa wananchi wake bila ya kutegemea sana upande wa pili wa Muungano.

MUWAZA inaamini kwamba vyombo vya ulinzi vitazidi kutumia hekima na busara ili kuepuka kuwa chanzo cha mtafaruku, na kwamba matukio yaliyopita siku za karibuni hayatokei tena siku za mbele.

MUWAZA inathamini kazi kubwa iliyofanywa na taasisi za kiraia hasa jumuiya ya UAMSHO ya kutoa elimu ya kiraia juu ya nafasi ya Zanzibar ndani ya mchakato wa katiba mpya. Tunapenda kuona kazi hiyo inaendelea kufanywa bila ya hamasa au jazba. Huu si wakati wa kujipatia umaarufu bali ni wakati unaohitaji mchango wa kila Mzanzibari. Ni vyema kupata ushauri na mashirikiano ya kila Mzanzibar.

MUWAZA inatoa wito kwa viongozi wa siasa, dini pamoja na waandishi kujiepusha na kauli za utatanishi zinazoweza kufitinisha au kutatanisha baina ya raia.

MUWAZA inapenda kuwatahadharisha Wazanzibar kuwa huu ni wakati wa kuendelea kuungana na kuwa na kauli moja ili kuipata Zanzibar tunayostahiki. Tujaribu kuziepuka mbinu chafu za wasiopendelea maelewano na mshikamano wetu katika kudai mamlaka ya nchi yetu. Ni vyema kukumbuka kuwa safari iliyo mbele yetu ni refu na itakumbana na vitimbakwiri vingi.

MUWAZA ingependa kuona Serikali ya Zanzibar inachukua hatua za makusudi kusikiliza maoni na wito wa raia wake juu ya suala zima la Muungano. Hatuoni kuwa ni jambo la busara kukaa kimya bila ya kutoa kauli yeyote kuhusiana na jambo hili.

Zanzibar kama mwenza wa Muungano wa Tanzania inahitaji kuwa na msimamo madhubuti unaoendana na matakwa ya wananchi wake juu ya mchakato wa katiba mpya. Tumesikia misimamo ya asasi za kiraia, vyama vya siasa, na hata Serikali ya Muungano (kupitia sheria ya katiba mpya) lakini bado hatujasikia msimamo wa Serikali ya Zanzibar.

Dr. Mohammed Z Salim,
Kaimu Mwenyekiti wa MUWAZA
June 3, 2012

Advertisements

About uamshozanzibar

Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislam, Zanzibar

Posted on June 3, 2012, in Uncategorized. Bookmark the permalink. Leave a comment.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: